Jumamosi 26 Julai 2025 - 20:13
Ayatollah Al-Udhma Sistani azitaka Nchi za Kiarabu na Kiislamu Kukomesha Janga la Ghaza

Hawza/ Katika kilele cha janga la kibinadamu linalozidi kuenea huko Ghaza, ambapo watoto na raia wasio na hatia wanahiliki kutokana na janga la njaa, Ofisi ya Ayatollah Al-Udhma Sayyid Ali Sistani imetoa tamko la dharura, ikiitaka jamii ya Kiislamu na jumuiya ya kimataifa kuwaokoa watu wa Palestina kutokana na mauti ya kimbari, huku ikionya kuhusu ukimya wa dunia mbele ya msiba huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya  Shirika la Habari la Hawza, kufuatia hali ya maafa ya kibinadamu inayowakumba Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza – hali ambayo imefikia kiwango cha njaa ya kutisha na kuongeza mateso chini ya kuzingirwa na kuvamiwa kunaoendelea – na baada ya takriban miaka miwili ya uharibifu na mauaji ya wasio na hatia wakiwemo watoto, wanawake na wazee, vilio duniani kote kwa ajili ya kusitishwa kwa janga hili vinazidi kusikika kila leo.

Kutokana na muktadha huu, Ofisi ya Ayatollah Al-Udhma Sayyid Ali Sistani, kwa mujibu wa msimamo wake thabiti kuhusu masuala ya Umma wa Kiislamu na kusimama pamoja na wanyonge, imetoa tamko likiitaka jumuiya ya kimataifa, hususan nchi za Kiarabu na Kiislamu, kukubali wajibu wao wa kimaadili na kibinadamu na kuchukua hatua za dharura kuwaokoa raia wasio na hatia kutokana na makucha ya njaa na mauti.

Tafsiri ya matini ya tamko hilo ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim

Baada ya takriban miaka miwili ya mauaji na uharibifu usiokoma, yaliyosababisha mamia ya maelfu ya mashahidi na majeruhi na kubomoa kabisa miji na makazi ya raia, siku hizi watu wanyonge wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha; hasa ukosefu wa chakula uliosababisha njaa ya kutisha ambayo imewaathiri hadi watoto, wagonjwa na wazee.

Ingawa kwa majeshi ya uvamizi hakuna kitu cha kushangaza zaidi ya ukatili huu wa kutisha – kwa kuwa wapo katika mwendelezo wa jitihada zao za kuwasambaratisha Wapalestina kutoka katika ardhi yao – lakini nchi za ulimwenguni, hususan nchi za Kiarabu na Kiislamu, zintarajiwa kuwa hazitaruhusu janga hili kubwa la kibinadamu kuendelea, bali zitumie jitihada zao zote kulikomesha na zitoe shinikizo kubwa zaidi kulazimisha utawala vamizi na waungaji mkono wake kufungua njia ili kupeleka chakula na mahitaji mengine ya msingi kwa raia wasio na hatia haraka iwezekanavyo.

Picha za kutisha za njaa inayo angamiza huko Ghaza zinazochapishwa na vyombo vya habari zinachoma dhamira ya kila mwanadamu aliye macho, na hata kuondoa ladha ya kula na kunywa kwa kila aliye na chembe ya dhamira, kama alivyosema Amirul-Mu’minin Ali (as) kuhusu kudhulumiwa kwa mwanamke mmoja katika ardhi za Kiislamu:
"Ikiwa Mwislamu atakufa kwa huzuni baada ya kushuhudia janga hili, basi si lawama kwake bali anastahiki kusifiwa."

و لا حول و لا قوه الا بالله العلی العظیم

29 Muharram 1447 H – sambamba na 25 Julai 2025 M

Ofisi ya Mtukufu Ayatollah Al-Udhma Sistani – Najaf Ashraf

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha